- · Asema msingi wa TAG ni kujitegemea
- · Mchungaji Mchodo amuahidi kuteka mji
Na Joseph H. Ongong’a
“Kila anayefanya kazi kama hii iliyofanywa na kanisa hili, Bwana ameahidi kumkumbuka, wachungaji epukeni kuwa bahari mfu, bali muwe watendaji wazuri kwenye maeneo yenu, mkikumbuka kwamba, Kanisa la Tanzania Assemblies of God, msingi wake ni kujitegemea na siyo kutegemea misaada kutoka kwa wazungu,” hayo ndiyo yaliyokuwa maneno ya Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, kati ya mengi aliyosema, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kanisa la Shekinah Temple, Mbagala Mgeni nani, iliyofanyika wiki iliyopita.
Askofu Dk. Mtokambali alisema kuwa, Kanisa la TAG kwa asilimia mia, linajengwa na wana TAG, wenyewe, na kama wakitokea wahisani wengine kutoka nje wanachukuliwa kama kunguru tu na wala hawapaswi kutegemewa kama ndio msingi wa maendeleo ya kanisa hilo.
Aidha Askofu Dk. Mtokambali ambaye alizindua Jengo hilo muda mfupi tu tangu alipoingi kwenye uongozi kwa awamu nyingine ya pili, alitumia fursa hiyo kuipongeza kanisa la Shekinah Temple, kwa kazi nzuri waliyoifanya wakishirikiana bega kwa bega na Mchungaji wao Samson Mchodo, kwa muda mfupi tu wa miaka minne tu tangu alipoanza huduma kwenye eneo hilo la Mbagala Mgeni nani.
Askofu ailiwataka Wachungaji wengine kufunguka na kuanza sasa kufanya kazi ya Mungu kwa kasi kubwa, wakipanua majengo yao, huku wakitambua kuwa, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ilikuwa ni kipindi cha kuweka msingi wa kazi, na sasa ni wakati wa kukimbia mchakamchaka. “Conference” imekwisha, sasa kazi imeanza na wakati wa kumulika tochi umekwisha, imesalia kupeana miraba na kukimbizana ili mwisho wa yote, Tanzania ivunwe kwa Yesu, na pia ni wakati wa makanisa kujaa na kuongezeka kwa kasi sana ndani ya miaka minne mingine ijayo,” alisema Askofu.
Alisema, pamoja na kutarajia mafanikio hayo makubwa, lakini pia hakuna kitu kizuri kinachozaliwa hivi hivi bila maumivu, na kama hautaji maumivu utaendelea kubaki kwenye maisha ya uduni mpaka Yesu atakaporudi.
Askofu Dk Mtokambali aliwahusia baadhi ya wachungaji na maaskofu waliohudhuria uzinduzi huo kutamani kuishi kama kanisa la Filadelfia, ambapo pamoja na mji huo kuwa na umaarufu sana lakini bado kanisa lililokuwemo na liliendelea kuwa na uvumilivu likitunza utakatifu wake. Aidha alisema kuwa, shauku ya Kanisa la TAG ni kubaki kama kanisa la Filadelfia, ambaoyo maana yake ni upendo wa Kidugu.
Mtumishi huyo wa Mungu alimpongeza Makamu wake Askofu Dk. Magnus Mhiche, ambaye ndiye mwanzilishi wa tawi hilo, kwa kazi kubwa aliyoifanya wa kufungua matawi mengi zaidi katika ukanda huo wakati alipokuwa Akofu wa jimbo la Mashariki.
Akisoma risala mbele ya Mgeni Rasmi, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Mmisionari Samson Mchodo alisema, kanisa hilo la Shekinah Temple, lilianzishwa Machi 2000 , ikiwa chini ya Mchungaji Samwel Mwita, ambaye kabla ya kupewa majukumu mengine alilichunga na kulikabidhi likiwa na waumini 72 mwaka 2008 na hadi kufikia sasa lina zaidi ya waumini 260, watu wazima na watoto.
Mchungaji Mchodo alisema, ili ujenzi wa jengo hilo liweze kukamilika, lilihitaji shilingi milioni 41, ambapo katika utekelezaji wake, tayari wametumia kiasi cha shilingi milioni 26 sawa na asilimia 70, ya gharama zote, kiasi kinachohitajika bado ni kama milioni 15, sawa na asilimia 30.
Alisema kuwa, kanisa la TAG Shekinah Temple, linayo malengo ya muda mfupi na muda mrefu katika kufikia utekelezwaji wa mpango mkakati wa miaka 10 ya mavuno, ambapo alifafanua kwamba, ili kufikia maono na malengo hayo, sanjari na kuwahudumia jamii kiroho na kimwili, kanisa linatakiwa kupata kiwanja kikubwa kitakachotosha kujenga Jengo kubwa litakaloweza kuchukua zaidi ya watu 300, kwa wakati mmoja, na kujenga kituo kitakachohudumia watoto.
Mchungaji Mchodo aliahidi kufanya kazi kufa na kupona kwa manufaa ya kanisa na kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Kumi ya Mavuno, kwa kasi ya aina yake kwa kipindi cha miaka minne mingine ijaya. “Askofu leo nakuahidi mbele yako kuwa sasa kazi imeanza na nitachapa kazi bila kuhofu kitu chochote ili kujenga ufalme wa Mungu,” alisema Mchungaji mchodo
Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali aliongoza watu kwenye harambee, ambapo yeye pamoja na michango mingine ambayoaliishawahi kuto, aliahidi tena kuchangia kazi hiyo kwa shilingi milioni 2.5, na katika harambee hiyo zilipatika pesa taslimu 425,000/= na ahadi ya shilingi 5,780, 000, zilipatikana.
Ukitaka kupata ushauri au unamchango wowote kwa ajili ya huduma hiyo, unaweza kuwasiliana na mchungji kiongozi wa kanisa hilo kwa simu namba: 0756576609
0 comments:
Post a Comment