Vita vya
wafanyabiashara(machinga) na Serikali ni machungu ya mwaka 1973, 74
Kwa miaka 50 sasa tangu uhuru wa Tanzania, mwaka 1961,
watanzania wamepitia katika mifumo ya uongozi wa Viongozi wanne,
ambao kila mmoja katika harakati zake za kutaka kuwapendezesha wananchi wake,
alichomoza na kauli mbiu na mikakati
yake ambayo kwa sehemu ililenga na
kukusudia ama kuleta mbadiliko ambayo aliona kuwa huenda yalikuwa ni mapungufu
wakati wa uongozi uliopita kabla yake, au kuja na jambo jipya.
Hayati Mwalimu JK Nyrere, yeye baada ya kuwatoa wananchi wa
Tanzania kutoka kwenye makucha ya ukoloni ya Waingereza Mwaka 1961, atakumbukwa
sana na mpango wake wa Vijiji vya Ujamaa vya mwaka
1973, 74, Mwingine aliyepokea kijiti hicho mwaka1985 – 1995 ni Mzee Ally Hassan
Mwinyi, aliyeibuka na Ruksa, hadi akabatizwa “mzee wa ruksa,” miaka kumi baadaye,
1995 – 2005, alifuatia mwingine na sera yake ya “Uwazi na ukweli,” naye siyo
mwingine ni rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.
Rais mwingine
aliyefuata baada ya hapo ambaye ndiye yupo madarakani hadi sasa akijaribu kukusanya mawazo yote ya wenzake
watatu, waliomtangulia, ili kuyaweka sawa mawazo yao, huku akikutana na
changamoto nyingi ni; Jakaya Mrisho
Kikwete, na kaulimbiu zake tatu, Hari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya, alipofikia
nusu ya mhula wa utawala wake, nadhani alipoona pengine kuna mafanikio kidogo
akachomoza tena na; “Hari mpya, Nguvu mpya na Kasi zaidi,” na kama haitoshi
akaja na “Maisha bora kwa kila mtanzania!”
Baadhi ya watanzania waliozaliwa katika kipindi cha nyuma,
kabla ya miaka ya 70, watakumbuka shuruba, adha na machungu waliyokutana nayo, wakati
wa kuundwa kwa Ujamaa vijijini, ambapo jamii waliokuwa wakiishi kwenye maeneo
yao mashambani (scattered areas) wakati huo, kabla na wakati wa uhuru 1961, walihamishwa na
kulundikwa pamoja kama vile uyoga, kwa kile kilichoelezwa kwamba ni kutengeneza
mfumo mzuri wenye miundombinu utakaowezesha kutoa huduma za muhimu kwa wepesi.
Kwa mtazamo wangu mimi, mpango wa Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, haukuwa mbaya, ila tu ulikosa uendelezaji (implementation),
kwani wakati huo aliposhika madaraka kutoka kwenye makucha ya wakoloni,
Waingereza, hakukuwa na vijiji, kata, Tarafa wala miji mikubwa kama Dar es Salaam, tuliyonayo hivi
sasa.
Jamii ya watu waliishi
maporini tena shughuli zao kubwa ilikuwa
ni uwindaji, kufuga na baadhi walijishughulisha na uvuvi, mfano mzuri ni jamii
ya Watindiga, Wamasonjo, Wadaatoga, Wabarbaig na wanao fanana nao ambao hadi sasa mpango wa
kuwatowa maporini haukuweza kuwafikia ipasavyo, japo kuna mikakati ule wa mwaka
1973, 74 inayoendelea kutekelezwa kwao hadi sasa.
Kwa mtazamo wangu, mpango wa Hayati Nyerere, wa uundwaji wa
Vijiji vya Ujamaa (socialist Villages), ambao baadae ulizaa ujamaa na kujitegemea (Self Reliance),
ulitiliwa mkazo na kiongozi aliyekuwa
Waziri wake mkuu wakati huo, Hayati Rashid Mfaume Kawawa, kwa hari kubwa sana
na utekelezwaji wake ulifanikiwa japo kwa maumivu makubwa sana.
Katika kipindi hicho,
nilikuwa na umri mdogo sana, sikuweza kuona na sikuwa na kumbukumbu ya kutosha
kuweza kujua yaliyojiri wakati huo, lakini ninao ujasiri wa kuelezea haya
kutokana na historia niliyosimuliwa na
wazazi wangu hao kuhusu mpango huo, wakati nilipoanza kupata ufahamu wa kutosha
wa kutambua mema na mabaya.
Baadae nilipopelekwa kuanza shule ya msingi
miaka ya 19 baada ya uhuru, kwa sehemu nilionja vuguvugu la mpango wa vijiji
vya ujamaa, kwani bado mjenzi mkuu wa mpango huo Rais wa awamu ya kwanza hayati
J.K. Nyerere, alikuwa bado anashika hatamu na wakati huo alihakikisha kwamba,
kile alichokiaanzisha kinatekelezwa barabara. “Walilazimika kuhama na watoto,
kuku, vitanda na mifugo bila kujua wanakokwenda na kuishia maporini ”.
Kwa ujumla
operesheni vijiji ilisababisha mateso yasiyoelezeka. Wajawazito
walijifungulia porini, watu waliliwa na wanyamapori na kuumwa na wadudu achilia
mbali kunyeshewa na mvua wakiwa wanalala chini ya miti.
Haikushangaza
kwamba mwishoni mwa mwaka 1974, takwimu zilizopo zaonyesha kuwa vijiji 5,000
vilikuwa vimesajiliwa vikiwa na jumla wakazi millioni 2.5.
Kwa ujumla wake
kati ya mwaka 1973 na 1975 jumla watu milioni 9 walikuwa wamehamishwa, wengi
wao kwa nguvu, kutoka vijiji vyao vya asili na kulundikwa kwenye vijiji vya
ujamaa mithili ya wakimbizi. Mpango wa serakali ukiwa ni kila
kijiji kukaliwa na familia takriban 250.
Ilipofika mwaka
1979, serikali ilitangaza rasmi kwamba watu milioni 14.9 sawa na asimilia
87 ya Watanzania wote, walikuwa wamehamishiwa kwenye “vijiji vya ujamaa”
vipatavyo 8,299.
Athari za
operesheni vijiji siyo kwamba malengo yote hayakufikiwa bali watu walirundikwa
kwenye maeneo ambayo hayakuwa yamefanyiwa utafiti kuwa yanafaa kwa makazi.
Matokeo yake uzalishaji wa mazao yote ya chakula na biashara ulianguka.
Msimu wa 1974/75
ulikuwa ni msimu wa njaa kubwa kiasi cha watu kuponea unga wa njano kutoka
Marekani. Viwanda vya korosho vilivyokuwa vikijengwa wakati huo kwa mkopo wa
Benki ya Dunia, vilibakia magofu hadi leo baada ya mashamba ya korosho kugeuka
mapori baada ya watu kuhamishwa.
Sera ya Azimio la
Arusha ya Mwaka 1967, ililenga kuendeleza mpango huo ambao ulianza kazi baadae
mwaka 1973, 74 ambapo wazazi
walihamasishwa kulima katika mashamba ya
vijiji vya ujamaa, halikadhalika wanafunzi nao walikwenda kupalilia
katika mashamba hayo. Kingine nilichokishuhudia ni pamoja na adhabu waliyopata
wale waliojitenga kushirikiana ama kutohudhuria katika mashamba ya ushirika,
walichapwa viboko na wengine walichukuliwa mifugo yao kama moja ya fidia.
Wazee waliokuwepo wakati huo, ambao wengi wao ni vikongwe
sasa, pamoja na watoto wao ambao sasa ni watu wenye umri mkubwa, watakubaliana
nami kuwa, walipitishwa katika kipindi kigumu, ambacho walitakiwa kufanya
maamuzi magumu, ambayo kwa sehemu fulani hawakukubaliana nayo kabisa, baadhi ya
watu walipoteza maisha yao kwa kuliwa na simba, wengine kutokana na wingi wa
watu(population), walikufa kwa magonjwa baada ya kuhamishwa na kulundikwa
katika sehemu moja pasipo kujengewa nyumba wala uangalizi wowote wa msingi
Wajenzi wazuri wa hoja
na wanafalsafa wanasema: “hakuna jambo zuri linalotendeka popote posipo kuwa na maumivu,” usemi huo unafanana
sana na ule usemao; “magomvi ni chanzo
cha maendeleo,” (Crisis is the source of development).
Wakati wa utekelezwaji wa mpango huo, wengi walimchukia sana
Mwalimu na waziri wake mkuu aliyekuwepo awamu hiyo, hayati Mfaume Kawawa,
sawasawa na ilivyo kwa baadhi ya viongozi wanaojaribu kutekeleza mpango wa
kuwaondoa wafanyabiashara kwenye maeneo yao waliyoyazoea na kuwaacha kama
yatima bila kuwaelekeza mahali pengine
panapowafaa kwa biashara, wanavyo pambana kufa na kupona kupinga kuondolewa
kwenye maeneo yao.
Siyo kwamba napingana kabisa na mpango huu wa Serikali,
ninacho kifahamu hiyo ni moja ya utekelezaji wa sera zao na kutimiliza ahadi
walizowaahidi wananchi wao, wakati wa kampeni za uchaguzi wa utekelezwaji wa
mpango wao mrefu wa kuwaletea maendeleo.
Pamoja na yote hayo lakini nadhani kuna sababu ya kurejea nyuma kwenye mpango wa misingi
ya Mwalimu Nyerere wa Mwaka 1974, uliolenga kuwaondoa watu katika maeneo yao ya
shamba (scattered area) na kuwalundika
sehemu moja kama uyoga(vijiji vya ujamaa), na baadaye watengeneze vijiji, miji
na jiji kama tuonavyo leo.
Baada ya mpango huo kukamilika japo kwa shida na maumivu
makubwa, sasa jamii ya watanzania waliishi kama ndugu moja, jamaa moja, na hata
nyumba zao zinavyoonekana katika miji mikubwa na midogo, vijiji, kata, tarafa,
wilaya na mikoa na katka sehemu mbalimbali hapa nchini ni kirafiki sana, nyumba
zimsogeleana kama uyoga uliojiotea pasipo plani yoyote, sijui kama serikali
walifikiria kwa kina kwamba hali hii ingekuwa hivi baada ya miaka kadhaa.
Kuna wakati Serikali inafanya maamuzi mengine ambayo
yanapingana sana na mipango yao hasa yanayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi
wao. Katika ujenzi wa hoja hii, hivi kuna sababu gani kwa serikali hiyo moja kuwatoa
watu wake maporini na kuwaleta kuishi
sehemu moja wakati huo huo, baada ya muda wanapanga kuwaondoa kutoka
sehemu moja(mijini) bila kuelekezwa wapi pa kwenda.
Mpango wa hayati Mwalimu Nyerere, ulilenga hasa kuwatoa watu
katika utengano wa makabila na kuwaleta kuwa jamii moja inayopendana,
inayofanya kazi kwa ushirikiano na kuondokana na vita vya koo na makabila,
ambayo kwa sehemu imefanikiwa, japo katika baadhi za sehemu kama vile Mkoa wa
Mara, alipotoka Mkuu huyo wa nchi wilayani Tarime, hali bado ni tete, hii
nadhani kwa Tarime mpango huo ulikuwa ni mgumu kufanikiwa sana kutokana na andiko lisemalo; “Nabii hapati heshima
nyumbani kwake.”
Ukitaka kuamini kuwa Serikali inaendeleza mpango wa Mwalimu Nyerere, kwa
mtazamo tofauti, tazama yanayotokea hivi sasa katika baadhi ya miji mikubwa
kama vile Dar es Salaam, Mbeya, Arusha
na kwingineko, kwa kile wanachodai kuwa wanatekeleza mipango yao ya muda
mrefu(long plan), ya kuleta maendelea hasa mabarabarani, ambapo watoto, wajukuu
na vitukuu wa wazazi waliohamishwa kutoka maporini na kukusanywa katika miji,
wanarejeshwa tena kukumbukia machungu na mateso yaliyowapata wazazi wao mwaka wa 1973,74.
Nadhani wakati wa uundwaji wa mpango huo wa hamisha watu kwenye
maeneo yao ya mashamba, hakukuwepo na wataalamu
wa kutosha wa kuchambua faida na hasira, na ndiyo maana katika mpango wa
serikali wa kuwabomolea watu na kuwahamisha kutoka kwenye makazi yao, na sehemu
wanapojitafutia riziki mijini, kwa ajili ya upanuzi wa barabara inaleta
mtafaruku mkubwa.
Kwa mtazamo wangu najisikia haya kusema serikali haiko
makini(smart) katika kupanga mambo yake, na kuwa wanapaswa kuwajibika kwa
wananchi wake katika maamuzi yote yanaamuliwa wakati huu, hebu fikiria nyumba
zile zilizojengwa na NSSF kama uyoga, kule Dodoma, utakuja sikia baada ya miaka
kadhaa tu, zinabomolewa tena kwa ajili
ya aidha upanuzi wa barabara ama kwa jambo fulani, sasa tujiulize serikali
inapopanga mipango yake wanakuwa hawana maono ya baadae ama wanamakusudi mabaya
kuwatesa tu raia wake?
Wakumbuke kwamba yale wayafanyayo wakati huu wa sasa,
unawasababisha raia kukosa imani nao, na ndio maana wanawekwa katika mazingira
magumu wakati wa utekelezaji wa mipango yao ambayo kwa sehemu inaonekana
kulenga kuleta maendeleo kwa taifa.
Nadhani kama wangekuwa ni watu makini, haya majengo makubwa
na ya heshima ya serikali yangejengwa kwenye maeneo yaliyo wazi ambayo
hayajakaliwa na watu, ndipo watangaze mpango wa bomoabomoa au hamisha, badala
ya kuwahamisha kwa mabavu pasipo mpango maalum na yakinifu unaowaacha wakiishi
katika mahema, huku wakiteseka bila mahitaji muhimu ya lazima; mfano mzuri
Mabwepande.
Kisaikolojia baada ya Vjiji vya Ujamaa mwaka 1974, watanzania
sasa wamejijenga kuishi kimjini mjini,
maisha yao yote na shuguli zao zinazowaletea kipato zinategemea penye
mkusanyiko wa watu, wanategemeana kila mmoja, na ndio maana ni vigumu sana
kuwaondoa na kuwapeleka kwenye mazingira mapya. Mtu mmoja aliwahi kuniambia;
“Huwezi kuniondoa mashambani ukanileta mji, halafu unitangazie kunirudisha
nilikotoka sikubali hata kidogo.”
Yale yanayowapata wakazi wa miji ya Dar es Salaam, Mbeya, nk,
yasije yakawapata wenzetu wanaoishi porini sasa, Wadaatoga, Wamasonjo,
Watindiga, na Wahadzabe. Na shauri wajengewe
kwanza maeneo na kuwekewa miundombinu imara ndipo mpango wa kuwahamisha kwenye
maeneo waliyoyazoea ufanyike, la sivyo waachwe waendelee kuponda maisha yao
kama walivyo zoea maporini.
0 comments:
Post a Comment