Mwamunyange:Tanzania haitaingia Vitani na Malawi
Na mwandishi wetu
WIKI moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema Tanzania haina mpango wa kupigana na Malawi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange amerejea kauli hiyo na akisisitiza kuwa Tanzania haitaingia vitani na nchi hiyo.
Akiwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika (Sadc) mjini Maputo Msumbiji, Rais Kikwete alisema kuwa uhusiano wa Tanzania na Malawi utabaki kama ulivyo na diplomasia zaidi itatumika.
Jana katika hafla ya kuwaaga Meja na Mabrigedia Jenerali, kwenye Kambi ya Abdallah Twalipo, Mwamunyange alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kuwa Tanzania itaingia kwenye vita na Malawi.
“Suala la mgogoro huu, linazungumzika na wahusika wanalifanyia kazi kwa karibu,” alisema Mwamunyange.
Wakati akisema hayo, kuna taarifa kuwa baadhi ya vikosi vya jeshi vimesogezwa kusini mwa Tanzania licha ya kuwa msisitizo kuwa hakuna mpango wa mapigano.
Mbali na hayo, katika hafla hiyo ya jana walioagwa ni Meja Jenerali, Nicholas Miti, Festo Ulomi, Samuel Kitundu na Said Kalembo ambaye mara ya mwisho alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Wengine ni Brigedia Jenerali Matata Magwamba, Grayson Idinga na Loth Kilama ambao wamemaliza utumishi wa jeshi wa muda usiopungua miaka 35.
Akizungumza kwa niaba ya wastaafu hao wa jeshi, Kalembo alisema, “Ninawataka Watanzania kudumisha upendo na mshikamano, kufanya kazi kwa kujituma ili kujenga taifa.”
Aliwataka wale wanaoingia jeshini kuwa na nidhamu ya jeshi kwa kuwa wana jukumu kubwa la kulinda mipaka ya nchi kwa jumla.
Hata hivyo, alipotakiwa na waandishi wa haba
ri kuzungumzia mipango yake ya baadaye kama ataingia kwenye siasa, alisema, “Sifikirii hivyo, kwani ukiwa mwajeshi unakuwa na amri.”
0 comments:
Post a Comment