PATA HABARI/MAKALA ZA UHAKIKA

+255-767-402-396

Qatar imepewa saa 48 kutimiza wajibu

Nchi za kiarabu ambazo zimesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Qatar zimekubali kurefusha muda wa Qatar kutimiza masharti iliyowekewa. Kuwait ambayo ni mpatanishi katika mzozo huo, ilipendekeza Qatar ipewe muda zaidi kujaribu kufikia masharti iliyowekewa na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri ambazo zinaishutumu nchi hiyo kwa kuunga mkono ugaidi, madai ambayo Qatar imeyakanusha. Qatar sasa ina saa 48 kutimiza masharti iliyowekewa la sivyo huenda ikawekewa vikwazo zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani anatarajiwa kutoa tamko rasmi leo kuhusu hatua hiyo ya hivi punde kuhusiana na mzozo huo. Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Umoja wa falme za kiarabu, Bahrain na Saudi Arabia watakutana Cairo Jumatano wiki hii kujadili ni hatua zipi zaidi watazichukua dhidi ya Qatar. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye leo anaanza ziara ya siku tatu katika mataifa kadhaa ya kiarabu ametoa wito wa kufanyika mazungumzo muhimu kuumaliza mzozo uliopo akisisitiza Ujerumani haiegemii upande wowote katika mzozo huo.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments: