PATA HABARI/MAKALA ZA UHAKIKA

+255-767-402-396

Madhehebu ya dini yanavyosaidia Serikali kuleta maendeleo kwa jamii



  • ·      Kanisa la TAG ikiwa kinara wa mpango huo, imeonesha mfano wa kuigwa

Na Joseph Herman
SERIKALI ya Tanzania imekuwa ikisisitiza Mashirika binafsi ya kidini kushiriki katika kuleta maendeleo kwa jamii. Kanisa la Tanzania Assemblies of God imeitikia kwa ari, Mpango Mkakati wa miaka 10 umegusa Watanzania. Makala hii inafafanua.
Maendeleo makubwa ya kijamii na kiroho ya wazi yaliyojifunua kwa jamii na kwa waumini wa kanisa hilo, yamegusa mioyo ya watumishi wake na hivyo kumfanya Mungu na wapiga kura awarejeshe viongozi wakuu wa kanisa hilo kuendelea na awamu nyingine ya miaka minne ijayo.
Hivi karibuni kanisa hilo limefanya Mkutano wake mkuu wa kikatiba, mjini Dodoma katika ukumbi wa Chimwaga UDOM, ambapo katika mkutano huo Askofu Dk. Barnabas Mtokambali alipata ushindi wa kishindo wa 94% kwenye kuara za maoni, kuendelea kuongoza kanisa hilo kwa miaka minne mingine, huku asilimia sita zilizosalia, waligawana watumishi wengine waliotajwa kwenye nafasi hiyo ya juu.

Viongozi wa Ofisi Kuu ya kanisa la TAG, waliorejeshwa kwenye uongozi na kanisa hilo wakati wa uchaguzi Mkuu. Katikati ni Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Barnabas Mtokambali, kulia ni makamu wake Dk. Magnus Mhiche na kushoto ni katibu Mch. Ron Swai.

Wengine waliochaguliwa  kuendelea kuongoza jahazi la maendeleo ya kanisa hilo kwa miaka mingine tena ni pamoja na Makamu Askofu Mkuu, Dk. Magnus Mhiche aliyeshinda kwa asilimia 74,  huku mshindani wake Askofu Lawrence Kametta akipata asilimia 24.
Kwa upande wa nafasi ya katibu Mkuu wa kanisa hilo, Mchungjai Ron Swai, alichaguliwa tena kwa kishindo baada ya kupata 93% huku asilimia saba wakigawana watumishi wawili waliomfuata.
Kurejeshwa kwa viongozi hao, inatokana na maono ya Mpango Mkakati wa Miaka 10, waliyonayo, yanayoonekana dhahiri kutekelezwa bila maneno na kasi yao ya utendaji katika kuleta maendeleo ya kiroho na kanisa likishirikishwa ipasavyo  kutatua kero za jamii wanamotumika.
Hotuba ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo iliyosomwa mbele ya wajumbe zaidi ya 5000 waliohudhuria mkutano huo, ilieleza ukweli unaoonekena dhahiri kutekelezwa na kanisa hilo kwa jamii kwa muda wa miaka minne ya uongozi wao.
MAENDELEO YA JAMII
·       Ujenzi wa shule
Sehemu ya hotuba hiyo ilieleza;pamoja na maendeleo mengine ya kiroho, lakini kanisa hilo katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango  Mkakati wake wa miaka 10,  imelenga kugusa jamii kwa kujenga shule za Seminari kupitia idara zake saba, na kanda zake zote na tayari baadhi zimekamilisha utekelezaji wa mpango huo.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Faraja Siha Seminari, mchipuo wa Sayansi, wakionyesha kwa vitendo mafunzo ya elimu ya sayansi shuleni hapo

Kanisa hilo limejidhatiti kupunguza adha kubwa ya wanafunzi wanaofaulu kukosa nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na elimu ya juu, ambapo sasa tayari Shule ya Seminari ya Ebenezer inayosimamiwa na idara ya Vijana CAS, iliyoko Iringa inafanya vizuri.
Shule nyingine ambayo pia inaendelea kufanya vizuri ni ile inayosimamiwa na idara ya Wanawake wa Kanisa hilo (WWK), ya Faraja Seminari na ile ya kidato cha tano  na sita Faraja Siha.

Moja ya Jengo la kisasa la Shule ya Faraja Siha Seminari ilipo Moshi, inayomilikiwa na Idara ya wanawake wa kanisa hilo.

Mikoa mingine ambayo imelengwa na tayari ujenzi wamajengo ya shule unaendelea ni pamoja na Morogoro, Mwanza, Rukwa,Tabora, Singida, Bagamoyo na Loboisoti huko Manyara.
·       Vyuo vya Ualimu
Mradi wa Vyuo vya Ualimu, ni moja ya vielelezo tosha kwamba kanisa la TAG limejipanga ipasavyo kuondoa adha ya ukosefu waalimu katika shule mbalimbali hapa nchini.
Katika kukamilisha mradi huo, tayari majengo ya vyuo viwili vya Ualimu vimesimikwa huko Tanangozi Iringa na Himo- Kilimanjaro na vyuo hivyo vinatarajia kufanya udahili wa Wanafunzi Walimu mwakani na kila chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 200.
·       Uchimbaji visima vya maji safi vijijini
Mradi mwingine wa kijamii unaoendeshwa na kanisa hilo hapa nchini ni pamoja na ule wa uchimbaji wa visima vya maji safi na salama.
Hutuba ya Kiongozi huyo wa Kiroho ilieleza kwamba, lengo kubwa la uchimbaji wa visima hivyo vya maji safi na salama ni kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuondoa adha ya maji kwenye maeneo kame huko vijijini. Hadi sasa Imechimba visima virefu 43 ndani ya miaka hii minne, lakini katika mpango wao jumla ya visima 108 vimeishachimbwa.

Mkurugenzi wa miradi wa TAG, Askofu Dk. Magnus Mhiche akipampu maji wakati wa uzinduzi wa moja ya kisima cha maji kilichochimbwa na kanisa hilo. Mradi wa uchimbaji wa visima ni moja ya kusaidia serikali kufikia jamii hapa nchini.

Tayari katika badhi ya mikoa kadhaa hapa nchini mradi huo umekamilika na jamii inafurahia huduma inayofanywa na kanisa hilo  kubwa la Kipentekoste hapa nchini ikishirikiana na wamishenari wake.
Mikoa ambayo tayari imefaidika na mradi huo wa visima ni pamoja na; Dodoma, Singida, Simiyu, Manyara, Arusha na Mwanza.
Mikoa mingine inayostawi na visima hivyo ni pamoja na, Lindi, Mtwara, Rukwa na Morogoro.

·       Uanzishaji wa benki
Uanzishwaji wa Benki ya UWEZO FINANCIAL SERVICES iliyoko mbioni kukamilika, ni moja ya huduma ya kijamii inayogusa mioyo na hivyo kufanya  waumini wa kanisa hilo kuweka imani ya hali ya juu na viongozi wao katika kuwafikisha kwenye maendeleo ya juu zaidi.
·       Ujenzi wa vituo vya afya

Katika kuhakikisha kwamba afya ya jamii inalindwa ipasavyo TAG imetekeleza utaratibu uliotokana na sera ya serikali kutoa nafasi kwa jamii kuchukua majukumu zaidi kwa maendeleo yao katika kufanya maamuzi kuchagua mradi wa afya kwa kujenga zahanati zitakazotoa huduma hiyo kwa jamii.


Watumishi wa Mungu wa kanisa la TAG,wakiweka wakfu zahanati ya kisasa iliyojengwa na kanisa hilo mjini Dodoma

Kanisa la TAG halikuacha kuchungulia kwenye mradi wa huduma hiyo ya afya, na kwa utekelezaji wa Mpango huo, tayari zahanati ya kisasa imeanza kufanya kazi ndani ya Chuo cha Biblia cha Central Dodoma.

 Askofu Mkuu wa kanisa la TAG, Dk. Barnabas Mtokambli(katikati), akielekezwa jambo na baadhi ya madaktari wa zahanati hiyo.

Zahanati hiyo ya kisasa inayohudumia jamii kwa sasa ni kati ya baadhi zinazotarajiwa kujengwa na kanisa hilo maeneo kadhaa hapa nchini. 
·       Vyombo vya habari
Kanisa hilo la kiroho haliko nyuma kwenye tasnia ya habari kwani tayari kanisa hilo linamiliki Radio Ushindi FM, iliyoko Mbeya, Gazeti la Jibu la Maisha na  liko mbioni kuanzisha vingine pamoja na kuwa na kituo chake cha Luninga kitakachojulikana kama Victory TV hapa jijini.
HUDUMA ZA KIROHO
Kwa upande wa huduma za kiroho kwa watumishi wake na kwa waumini, kanisa hilo upanuzi wa vyuo vyake vya Biblia nchini kwa kujenga majengo ya kisasa na bweni ili kukidhi ongezeko la watumishi wake unaokuwa kwa kasi kubwa.


Hiki ni moja kati ya vyuo vya kiroho(Bible Colleges) inayomilikiwa na TAG huko Mbeya



Majengo hayo yaliyopanuliwa na kufanyiwa uboreshaji  ni pamoja na Mbeya Southern Bible College, Dodoma Central Bible College, Arusha, Mwanza- lake Victoria Bible College, Chuo cha Mtama Southern Bible College, Global Harvest.

Jengo la Bweni la kisasa la Chuo cha Biblia Dodoma, linalomilikiwa na kanisa hilo.




Kanisa la nchi la TAG kwa kurahisishia kazi ya utumishi watumishi wake, imewawezesha Maaskofu  wa Majimbo 33 nchi nzima, wakurugenzi wa idara, wakuu wa vyuo vya Biblia  na waangalizi kupata vyombo vya usafiri.
Watumishi wa Mungu wa kanisa hilo wakisubiri kupata vyombo vya usafiri kwa ajili ya kurahisisha utumishi wao

Kwa uapande wa Maaskofu wa majimbo, wakuu wa vyuo na Wakurugenzi wao wamepata magari wakati Waangalizi wa sehemu wa kanisa hilo wamepata pikipiki, zaidi ya pikipiki 400 zimegawanywa.


Askofu Mkuu wa kanisa hilo Dk. Barnabas Mtokambali, akizindua pikipiki zilizogawanywa kwa Waangalizi wa kanisa hilo



Katika mkutano huo TAG, pia ulifanyika uchaguzi wa kamati ya majimbo na sehemu za kanisa hilo, ambapo baadhi ya majimbo walipata viongozi wapya huku baadhi wakirejesha waliokuwepo awali.
Mapema Februari Mwaka huu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango(MB), akiwakilisha Bungeni  mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17, pamoja na mambo mengene lakini alitaja ushirikishwaji wa taasisi zisizo za Serikali kushiriki maendeleo ya jamii.
Dk. Philip katika hotuba yake hiyo  alisema: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17 yamezingatia maoni ya Wizara, Idara, na Taasisi za Serikali na Sekta binafsi. Masuala makuu ya maoni ya wadau yaliyojitokeza na kujadiliwa ni pamoja na: kuboresha miundombinu (maji, umeme na barabara) ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika viwanda nchini.
Madhehebu ya dini kushiriki katika harakati za kuleta maendeleo kwa jamii, kama kanisa la TAG ilivyoonesha ari ya kufanya ni kuitika wito wa serikali katika kuisaidia kuifikia jamii.


Share on Google Plus

About Unknown

0 comments: