Arusha, Novemba 09, 2012 (FH) – Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa
ya Makosa ya Jinai (ICC) wiki hii imetoa wito wa ushirikiano zaidi baina ya
nchi katika kushughulikia uhalifu uliofanywa nchini Libya, wakati mahakama moja
nchini Sweden imemshitaki raia wake mmoja mwenye asili ya Rwanda kwa mashitaka
ya mauaji ya kimbari.
SWEDEN
Mahakama yamshitaki raia wa Sweden mwenye asili ya Rwanda: Mahakama moja
nchini Sweden Jumatatu ilimshitaki raia wake mmoja mwenye asili ya Rwanda kwa
madai ya kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Mwendesha mashitaka
alisema kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa kuanzia Ijumaa ijayo na itakuwa
kesi ya kwanza ya aina hiyo kuwahi kusikilizwa nchini Sweden.Mtu huyo anadaiwa
kutenda uhalifu huo mkoani Kibuye, Magharibi ya Rwanda.
RWANDA
Ngoga aishutumu Uingereza jinsi inavyoshughulikia watuhumiwa wa mauaji ya
kimbari: Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, Martin Ngoga, Jumatatu iliishutumu
Uingereza kwa kutoshughulikia ipasavyo kesi za watuhumiwa wa mauaji ya
kimbari waliomo nchini humo.Alikuwa anajibu ripoti moja iliyoandikwa na vyombo
vya habari nchini Uingereza kwamba mnyarwanda mmoja, Modeste Kennedy,
anayedaiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, yuko nchini humo
akifanya kazi kama dereva wa taksi na kwamba hawezi kurejeshwa nchini Rwanda
kukabiliana na mashitaka dhidi yake kutokana na uzingatiaji wa haki za
binadamu.
ICTR
ICTR yapania kuhitimisha kesi zake ifikapo 2014: Maafisa wa Mahakama ya
Kimataiafa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Alhamisi walitangaza kwamba
mahakama hiyo itahitimisha kesi zake zote ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014
kulingana na muda uliopangwa. Maafisa hao wamesema hivi sasa mahakama hiyo ina
majukumu mawili muhimu.La kwanza, kuhitimisha usikikilza wa hatua ya awali ya
kesi ya mwisho na pia kukamilisha hukumu za kesi katika ngazi ya rufaa na
maamuzi mbalimbali yaliyosalia.
ICC
Mwendesha mashitaka wa ICC ahimiza ushirikiano: Mwendesha Mashitaka wa ICC,
Fatou Bensouda Jumatano ilitoa wito wa kushirikiana zaidi baina ya nchi na
mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa katika kushughulikia uhalifu
uliofanywa nchini Libya. Bensouda alikuwa anawasilisha ripoti ya nne juu ya
hali ya Libya, mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Alisema tangu
Machi 2011 mahakama hiyo ilipofungua upelelezi juu ya uhalifu wa kimataiafa
uliotendeka katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, imekwisha toa maombi ya kutaka
usaidizi 130 na mengi kati ya hayo hayajatekelezwa.
NI
© Agence Hirondelle
0 comments:
Post a Comment