PATA HABARI/MAKALA ZA UHAKIKA

+255-767-402-396

HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO MHESHIMIWA LEONIDA GAMA KWENYE MKUTANO WA MAOMBI YA KUOMBEA TAIFA TAREHE 22 NOVEMBER 2012




Mheshimiwa Baba Askofu Charles Gadi wa Good News for All Ministry toka Dar es Salaam, Waheshimiwa maaskofu na wachungaji na watumishi wa Mungu wa Mkoa wa Kilimanjaro mlioko hapa, wapendwa wachungaji na wanamaombi mliotoka Dar es Salaam, Viongozi wa Serikali wa mkoa na wilaya mliojumuika nasi hapa, Nawasalimu kwa jina la Yesu.
Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru Uongozi wa Huduma ya Good News For All Ministry na Watumishi wa Mungu hapa Kilimanjaro kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maombi haya maalumu kwa ajili ya kuombea Mvua, na kuombea Taifa letu kwa ujumla.
Nawashukuru pia kwa kuuchagua mkoa wangu wa Kilimanjaro kwa ajili ya kuendesha mkutano huu wa Maombi, na ninaamini mmeona kuna umuhimu katika ulimwengu wa roho kufanya hivyo na ninajua Mungu ataupendelea Mkoa huu na kuubariki kwa ajili ya maombi haya. Nina hakika mngeweza kuchagua mkoa wowote katika Tanzania hii katika kuendesha mkutano, lakini ilimpendeza Mungu na ninyi kuja Kilimanjaro.  Hivyo kwa niaba ya wana-Kilimanjaro nawakaribisha kwa moyo mkunjufu na jisikieni mko nyumbani.
Baba Askofu napenda kuwajulisha kuwa mkoa wetu wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa ambayo imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri ya kilimo, uoto mzuri wa asili, pamoja na vivutio vingi vya utalii bila kusahau Mlima wetu wa Kilimanjaro na mbuga ya wanyama inayouzunguka mlima huo na ile ya Mkomazi huko Same. Mkoa huu una uoto wa misitu mikubwa ya asili na ya kupandwa inayozunguka milima ya Upare mfano Msitu wa Shengena na misitu minene inayozunguka Mlima Kilimanjaro. Pia Mji wetu wa Moshi ni mji unaoongoza kwa usafi katika mazingira yake na ni kiungo kati Arusha ni miji ya Pwani ya nchi yetu, jambo linaloufanya kuwa na fursa nzuri za kibiashara na uwekezaji. Naomba nichukue nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji toka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika mkoa huu kwani ili kuzalisha nafasi za ajira kwa vijana wetu.
Baba Askofu, pamoja na mambo hayo mazuri ya mkoa wetu, kuna changamoto kubwa zinazoukumba mkoa huu na mikoa ya jirani, nazo ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti ovyo, uchomaji moto mapori na shughuli nyingine za Kibinadamu. Hilo limesababisha kuwepo na hali ya ukame katika maeneo mengi ya mkoa huu. Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na uhaba mkubwa wa mvua, jambo linalokwamisha sana shughuli za kilimo hasa yale maeneo ya uwanda wa chini. Katika wilaya kama Same, Rombo nk kumekuwa na upungufu wa chakula mara kwa mara, kutokana na upungufu huo wa mvua.
Pamoja na uharibifu huo wa Mazingira, kuna tatizo la ongezeko la Joto duniani, jambo linalotishia uwepo wa barafu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.  Hali hiyo ikiendelea itasababisha madhara makubwa katika mazingira yetu kwa ujumla na hata kupunguza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea Mlima Kilimanjaro, kwani barafu iliyo juu yake ni mojawapo ya vivutio, ikizingatiwa ndiyo mlima pekee ulio karibu na ikweta wenye barafu duniani.
Hivyo basi, tunaona kuwa maombi haya yamekuja kwa wakati wake kwani hata mvua zinazoanza kunyesha si za uhakika, kwani zinaweza kukatika wakati mazao ya vuli ndiyo kwanza yako nusu. Tunaamini kuwa Maombi haya yatasababisha kuwa na mvua za uhakika, na kuleta faraja na unafuu kwa wakulima wetu katika msimu huu wa vuli.  Pia tunaamini kuwa Mungu kupitia maombi haya anaweza kubadilisha hali ya hewa ha mkoa wetu ikarudi kama zamani.
Mheshimiwa Baba Askofu, napenda pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa ajili ya kujumuisha maombi ya kuombea amani katika nchi yetu, na mkoa wetu kwa ujumla. Sote si wageni kwa mambo yanayotokea sasa katika mikoa mbali mbali hapa, hususan vurugu za kisiasa na kidini ambazo zinaonekana kushika kasi katika siku za karibuni. Ni wajibu wetu kama viongozi wa Dini kutumia nafasi zetu kuelimisha waumini wetu umuhimu wa kuheshimiana, kuthaminiana na kuvumiliana ikiwa  ni pamoja na kujali dini na ibada za madhehebu mengine. Pia amani ya kweli ni tuzo ya Mwenyezi Mungu hivyo ni muhimu kumwomba kwa bidii ili nchi yetu ipate utulivu, na wanachi wetu waweze kupata wasaa mzuri wa kujiletea maendeleo yao. Amani ni kitu cha thamani sana, ambapo muda mwingi hutumika kuijenga, lakini kuibomoa ni jambo la muda mfupi, na uzoefu unatuonyesha kuwa nchi ambazo zimeharibu amani na utulivu wao, imewagharimu sana kuurudisha  na nyingine nyingi bado hazijaweza. Hivyo busara itumike sana kwenye kutatua migogoro ya kisiasa na kidini, ikiwemo uchaji wa Mungu na maombi.
Pamoja na maombi haya, naomba nitoe wito kwa wananchi wanaozunguka vyanzo vya mito ikiwemo misitu, watumie fursa hii kuitunza na kuepukana na ukataji wa miti ovyo, uchomaji moto mapori na kadhalika. Pia wananchi wapande miti ili kusaidia upatikanaji wa Mvua na kukinga vyanzo vya maji.  Ninaamini kuwa Mungu atasikia maombi haya na mvua itapatikana na mkoa wetu utapata neema kubwa.
Nawashukuru tena waandaaji wa mkutano huu, pamoja na ujumbe mzima toka Dar es Salaam kwa kufika kwenu na kutuunga mkono kwa njia ya maombi. Naomba nitangaze kuwa maombi haya yamefunguliwa na Mungu awabariki.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Mhe. Leonidas Gama
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments: