Rais Paul Kagame wa Rwanda, wiki hii amedai
kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ni fimbo ya
kisiasa iliyoanzishwa kuwapiga waafrika wakati pande za mwendesha
mashitaka na utetezi katika kesi inayomkabili Kiongozi wa waasi wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Thomas Lubanga wamekata rufaa
kupinga adhabu iliyotolewa.
RWANDA
Kagame aiita ICC fimbo ya kisiasa: –
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Alhamisi amedai kwamba Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yenye mamlaka ya kuwashitaki
watuhumiwa wa mauaji ya kimbari,uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya
binadamu, ni fimbo ya kisiasa iliyoanzishwa kwa lengo la kuwapiga
waafrika. Rais Kagame alisema hayo mjini Kigali wakati akizindua Mwaka
wa Mahakama wa 2012-2013 nchini humo.
ICC
Mwendesha mashitaka na mawakili wa utetezi wakata rufaa kesi ya Lubanga: Pande
zote mbili, za utetezi na mwandesha mashitaka katika kesi ya kiongozi
wa zamani wa wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),
Thomas Lubanga, zimekata rufaa kupinga adhabu aliyopewa mshitakiwa huyo
ya kifungo cha miaka 14 jela. Wakati mwendesha mashitaka anapinga adhabu
ya kifungo cha miaka 14 jela akitaka iongezwe, upande wa utetezi
unapinga vyote viwili, kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa.
Kesi ya Bemba yaahirishwa: Majaji
wanaosikiliza kesi ya utetezi ya Jean Pierre Bemba wamelazimika
kuisimamisha kwa kukosa mashahidi. Katika mkutano wa pamoja uliofanyika
Jumanne, majaji walisema shahidi aliyekuwa anatakiwa kuendelea kutoa
ushahidi wake mahakamani hapo Septemba 24, 2012, ametoweka huku shahidi
mwingine aliyetakiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake baada ya
mwenzake kuhitimisha,hakuweza hakupatikana.
WIKI IJAYO
ICC
Majaji kusikiliza ombi la Libya katika kesi ya mtoto wa Gaddafi: Majaji
wanatakiwa kuketi kwa siku mbili mfululizo kusikiliza maombi ya
serikali ya Libya inayopinga mahakama ya ICC kusikiliza kesi ya mtoto wa
kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, Saif al-Islam
Gaddafi.
ICTR
Mahakama ya Rufaa kusikiliza kesi ya mawaziri wawili wa zamani: Jumatatu
ijayo, Mahakama ya Rufaa ya ICTR itasikiliza kesi ya rufaa inayowahusu
mawaziri wawili wa zamani wa Rwanda, Justin Mugenzi na Propser
Mugiraneza.
Hukumu rufaa ya Gatete wiki ijayo: Mahakama
ya Rufaa ya ICTR, Jumanne ijayo, Oktoba 9, itatoa hukumu ya kesi ya
afisa mwandamizi wa zamani wa serikali nchini Rwanda,Jean Baptiste
Gatete.
NI/FK
0 comments:
Post a Comment