PATA HABARI/MAKALA ZA UHAKIKA

+255-767-402-396

MAJUMUISHO YA WIKI - SENOUSSI AREJESHWA LIBYA, HATMA YA KUMBUKUMBU ZA ICTR KUAMURIWA NA BARAZA LA USALAMA

Abdullah al-Senoussi
Arusha, Septemba 07, 2012 (FH) – Mauritania imemkabidhi kwa Libya, Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa nchi hiyo, Abdullah al-Senoussi huku John Hocking, Msajili wa Taasisi ya Kimataifa itakayorithi kazi za Mahakama za Kimataifa (MICT), amesema hatma ya mahali pa kuhifadhi kumbukumbu za Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) iko mikononi mwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
MAURITANIA
Senoussi arejeshwa Libya: Mauritania Jumatano wiki hii ilimkabidhi kwa Libya, Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa nchi hiyo, Abdullah al-Senoussi.Mtu huyo anahitajika na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) na Ufaransa.Alitiwa mbaroni Machi 17, 2012 alipokuwa anawasili katika uwanja wa ndege wa Nouakchott nchini Mauritania.Senoussi anatakiwa na Ufaransa ambako alihukumiwa pasipo kuwepo mahakamani adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kushiriki kwake katika kutungua ndege ya UTA nchini Niger mwaka 1989 ambapo watu 170 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo, walikufa. Nayo ICC ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Senoussi Juni 27, 2011 kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu unaodaiwa kufanywa Benghazi, nchini Libya.
KINSHASA   
Abdullah al-Senoussi
Utetezi katika kesi ya Bemba: Kesi ya kiongozi wa kundi la zamani la waasi la MLC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),Jean Pierre Bemba iliendelea kusikilizwa Jumatatu wiki hii. Shahidi, Octove Diabo, raia wa Gabon ambaye anadai kuwa ni mtaalamu wa masuala ya migogoro ya Kisiasa katika Afrika ya Kati amedai kwamba wanamgambo wa Bemba walikuwa na haki ya kuingilia mgogoro uliokuwepo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.Alisema wanamgambo wa MLC walikwenda kumsaidia Rais wa nchi hiyo, Ange Felix Patasse katika mapambano yake dhidi ya kundi la waasi wakati huo lililokuwa linaongozawa na Francois Bozize, ambaye ni rais wa sasa wa nchi hiyo.Upande wa mwendesha mashitaka ulimhoji shahidi huyo juu ya utaalamu alionao. Bemba anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita anaodaiwa kutenda kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
CTR
Baraza la Usalama kuamua hatma ya uhifadhi wa kumbukumbu za ICTR: John Hocking, Msajili wa Taasisi ya Kimataifa itakayorithi kazi za Mahakama za Kimataifa (MICT), Jumanne alisema hatma ya mahali pa kuhifadhi kumbukumbu za Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) iko mikononi mwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Rwanda imekuwa ikidai haki ya kuhifadhi kumbukumbu za ICTR baada ya kuhitimisha kazi zake kwa maelezo kwamba yenyewe ndiyo yenye haki ya kiasili ya kupokea kumbukumbu hizo kutokana na ukweli kwamba mauaji ya kimbari yalifanyikia nchini Rwanda.Wakati wa uzinduzi rasmi wa MICT, tawi la Arusha, Julai 2, 2012, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Rwanda, Martin Ngoga alisema wanahitaji majadiliano ya wazi katika masuala mbalimbali likiwemo hilo la uhifadhi wa kumbukumbu.
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma Jumatatu: Kesi inayomkabili kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (MLC), Jean Pierre Bemba itaendelea kusikiliza Jumatatu ijayo, Septemba 10, mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa kuendelea kupata ushahidi kutoka kwa mashahidi wa utetezi. Bemba anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.  
NI/FK
© Hirondelle News Agency
© Agence Hirondelle
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments: