Na mwandishi wa Idara ya habari Maelezo
WAKATI mazungumzo ya mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa baina ya Serikali za Tanzania na Malawi yakishindwa kupata suluhu, Malawi imetakiwa kusitisha shughuli za utafiti kipindi hiki cha kutafuta muafaka.
Hayo yamebainishwa katika mkutano wa wataalamu na viongozi kutoka serikali za nchi hizo baada ya kushindwa kufikia muafaka uliokusudiwa kuhusu eneo halali la mpaka unaozitenganisha.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao cha usuluhishi kilichohusisha timu za wataalamu na viongozi wa wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika juzi usiku mjini Lilongwe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, alisema Tanzania bado ina amini katika mazungumzo ili kufikia muafaka.
Alisema kuwa pamoja na sababu mbalimbali zilizotolewa na Malawi juu ya umiliki wa eneo lote la Ziwa Nyasa, msimamo wa Tanzania uko wazi kwa kuzingatia vielelezo vya historia vilivyoachwa na wakoloni na sheria za kimataifa kuhusu mpaka kuwa katikati ya ziwa hilo.
Membe alisema kuwa licha ya Serikali ya Malawi kuonesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo, viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika juzi usiku wameamua kuunda timu za wataalamu.
“Licha ya kuwasilisha vielelezo kuonesha uhalali wa mpaka, hatukuweza kufikia muafaka, tumefika mahali pa kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu zitoe mapendekezo ya nini kifanyike, maana kuna kila dalili kwamba sisi wenyewe tutashindwa kuendelea zaidi,” alisema.
Alisema kuwa wataalamu kutoka Malawi na Tanzana watakutana Septemba jijini Dar es Salaam ili waweze kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwapata wasuluhishi wa mgogoro huo pamoja na faida na hasara ya njia watakazozipendekeza.
Membe aliongeza kuwa, timu za wataalamu zitakazoundwa zitatoa mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa marais wa nchi hizo katika kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa mgogoro huo, ikiwemo kumtafuta msuluhishi au kwenda kwenye mahakama ya kimataifa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraimu Chiume, alisisitiza kuwa licha ya mgogoro huo kuhitaji busara zaidi, bado serikali yake inaamini kuwa mpaka kati yake na Tanzania uko upande wa mashariki mwa Ziwa Nyasa na unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
Alisema kutokana na unyeti wa suala lenyewe na eneo hilo pamoja na historia ya nchi yake, anapenda kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili wananchi wa nchi mbili waweze kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
“Ni matumaini yangu mkutano wa Dar es Salaam utakaofanyika Septemba utazaa matunda ili suala hili lipatiwe ufumbuzi, na ikiwezekana tupate msaada wa sheria za kimataifa kwa sababu suala hili liko kisheria zaidi,” alisema Chiume.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri Membe na makatibu wakuu, Patrick Lutabanzibwa (Ardhi), John Haule (Mambo ya Nje) Waziri wa Ardhi, Prof. Anna Tibaijuka na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Patrick Tsere.
*KAMATI KUU YATOA TAMKO KUWAPONGEZA MAWAZIRI WALIOWAWAJIBISHA WATENDAJI WA MASHIRIKA YA UMMA
Na Salesi Malula
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CC), imewapongeza mawaziri kwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji wanaotuhumiwa kwa vitendo vya matumizi mabaya ya ofisi za umma wakiwamo wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kuwataka waendelee na kasi hiyohiyo.
Pongezi hizo za Kamati Kuu zimetolewa baada ya kikao chake kilichofanyika Ijumaa iliyopita na zimekuja baada mawaziri kadhaa kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya watendaji walio chini ya wizara zao kwa tuhuma mbalimbali.
Mawaziri waliowachukulia hatua watendaji ni pamoja na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda.
Juzi, Kamati Kuu iliipongeza Serikali kwa kutekeleza maagizo yake ya kutaka ichukue hatua dhidi ya watendaji waliohusishwa katika ubadhilifu katika mashirika ya umma.
“Kamati Kuu inawapongeza mawaziri walioanza kutekeleza maagizo hayo kwani mwisho wa siku maisha bora kwa kila Mtanzania yatawezekana,” ilisema taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Kamati Kuu ilieleza katika taarifa yake kuwa ipo haja ya kuwachukulia hatua watendaji wakuu wa mashirika yaliyohusishwa na ubadhirifu mbalimbali na kwamba kitendo hicho cha mawaziri hao ni kutekeleza agizo lake.
Mei 17, mwaka huu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Kigoda alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kuyapa zabuni kampuni hewa za ukaguzi wa magari kabla hayajaingia nchini.
Muda mfupi baadaye, Juni 5, mwaka huu, Dk Mwakyembe alimsimamisha kazi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi kutokana na tuhuma mbalimbali.
Hivi karibuni, pia Dk Mwakyembe alisimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, wasaidizi wake wawili na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo kupisha uchunguzi wa wizi wa vitu mbalimbali yakiwemo makontena 40 ya vitenge katika Bandari ya Dar es Salaam.
Pia aliwasimamisha kazi Meneja wa Kituo cha Mafuta ya Ndege Kurasini (Kurasini Oil Jet - KOJ), Meneja wa Kituo cha Mafuta JET na mhandisi wa mafuta wa kituo hicho, baada ya kubainika kuwepo kwa wizi wa mafuta.
Waziri Kagasheki kwa upande wake, alimfukuza kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Obeid Mbanga kwa kashfa ya kusafirisha wanyama kwenda nje ya nchi.
Julai 14, mwaka huu, Bodi ya Tanesco ilimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando ikielezwa kuwa ni maelekezo ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo ili kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi yake.
Mbali na kupongeza kazi hiyo, pia CC ilizungumzia mgogoro wa Tanzania na Malawi. Kuhusu hilo, Nape alisema Kamati Kuu imewatahadharisha wanasiasa na vyombo vya habari vinavyochochea vita na uhasama kati ya nchi hizo mbili.
“Kamati Kuu imetaka suala hilo kuiachia diplomasia ichukue mkondo wake na Serikali iushughulikie na kuumaliza mgogoro huo,” alisema Nape.
Pia, ilipokea taarifa ya maendeleo ya uchaguzi ndani ya chama na kusema imeridhishwa na maendeleo hayo ya uchaguzi na kuagiza kila kikao husika kihakikishe haki inatendeka hasa katika uchujaji wa majina.
Nape Aikomalia Chadema
Akataa kuomba radhi, asema tuhuma atazithibitisha mahakamani, Amtaka Dk. Slaa kuandaa bilioni 3 na shilingi moja. Ni kwa kudai CCM inaingiza silaha nchini.
Na salesi malula.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amewataka Chadema kwenda mahakamani haraka badala ya kusubiri kuombwa radhi kama walivyotaka ili kusafishwa dhidi ya madai ya chama chao kupewa mabilioni ya fedha na mataifa tajiri.
Aidha amemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbrod Slaa kuiomba radhi CCM la sivyo itamburuza mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja, kwa kuituhumu uongo kwamba imeingiza silaha kutoka nje ya nchi tena bila kulipia ushuru.
Nape alisema hayo leo Agosti 27, 2012, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba mjini Dar es Salaam.
"Bila shaka mmesikia jana Chadema wakinitaka niombe radhi au wananipeleka mahakamani kudai fidia ya sh. bilioni 3, kwa madai eti nimesema Chama hicho kinapata mabilioni ya fedha kutoka kwa mataifa tajiri. Mkubwa hatishiwi nyau, nawataka waende haraka mahakamani wala wasisubiri hizo siku saba", alisema Nape.
Alisema, CCM inao ushahidi wa kutosha kuhusu madai aliyotoa Nape dhidi ya Chadema na kwamba huyo tayari kutoa uthibitisho huo mahakamani badala ya kuomba radhi.
"Nadhani wakienda mahakani itapendeza zaidi maana huko ndiko pazuri kutoa uthibitisho kuhusu tuliyosema, na ninawahakikishieni tukishathibitisha na Msajili wa Vyama akaupata uthibitisho huo chama chao kinafutwa", alisema.
Kuhusu CCM kumburuza Dk. Slaa mahakamani, Nape alisema, ameshawaagiza wanasheria wa Chama, kuandaa barua ya kusudio la mashitaka hayo, na Dk. Slaa atapelekewa ili aamue kama ataomba radhi au atakuwa tayari kwenda mahakamani.
"Wakati wanakwenda mahakamani, Chadema wamwambie babu yao ajiandae kuomba radhi au kuburuzwa mahakamani kuilipa CCM fidia ya sh. bilioni 3 na shilingi moja kwa kuizushia CCM uongo kwamba inaingiza silaha nchini tena", alisema Nape
0 comments:
Post a Comment