Salesi Malula na Joseph Ongong’a
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesitisha kwa muda mikutano yake iliyotarajiwa kufanyika mkoani Iringa.
Mikutano hiyo imesitishwa hadi baada ya kumalizika kwa Sensa ya Watu na Makazi inayoendelea nchini kote.
Uamuzi huo umekuja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, kuwaomba kufanya hivyo kwa masilahi ya taifa.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa, alisema walipigiwa simu juzi usiku na IGP Mwema akiwaomba kusitisha operesheni Sangara hadi baada ya kumalizika kwa Sensa ya Watu na Makazi mwishoni mwa mwezi huu.
Dk Slaa, alisema walitarajia kufanya mkutano na maandamano mkoani Iringa leo, lakini shughuli hiyo ya kisiasa haitakuwapo kwa sababu ya Sensa.
Hata hivyo, Dk. Slaa alisema baada ya kumalizika kwa Sensa, hawatakubali vikwazo vyovyote, badala yake wataendelea na mikutano yao kama kawaida.
“Sisi kama CHADEMA tuna taratibu zetu za kufanya shughuli za chama kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa.
“Kwa hiyo, kitendo cha kuzuiwa kutofanya mikutano na maandamano, tumekubaliana na ombi hilo, baada ya hapo tutaendelea na mikutano yetu.
“Kama ni uvumilivu tumeufanya kiasi cha kutosha lakini sasa uvumilivu huo huenda ukafika mwisho na hatua itakayofuata itakuwa si nzuri.
“Tumekubali kuahirisha japokuwa tunaingia gharama kubwa kwani msafara wa Operesheni Sangara una viongozi wasiopungua 70 kutoka mikoa mbalimbali pamoja na waandishi wa habari, kwa hiyo unapoahirisha ziara maana yake unaingia tena kwenye gharama zingine ambazo hukuzitarajia,” alisema.
Akizungumzia kifo cha mkazi wa Morogoro aliyedaiwa kupigwa risasi na askari polisi wakati walipokuwa wakidhibiti maandamano, alisema tukio hilo limewasikitisha kwa kuwa hawakulitarajia.
“Tukio lililotokea Morogoro kwa mtu kupoteza maisha limetusikitisha sana kama wana CHADEMA, tunaondoka mkoani hapa tukiwa na huzuni kubwa kwani polisi wamekuwa wakiendelea kumwaga damu za wananchi bila sababu za msingi.
“Lakini, ninachoweza kusema ni kwamba, pamoja na vitisho vilivyotolewa na Jeshi la Polisi, bado maelfu ya wananchi walijitokea katika mkutano huo ili kuonyesha jinsi tunavyokubalika.
0 comments:
Post a Comment