Mwaka 2010, taifa letu lilishuhudia tena uchaguzi mkuu mwingine
ulioshirikisha vyama vingi. Katika Jimbo la Arusha Mjini, Godbless
Jonathan Lema (ambaye hapa ni mwomba rufaa katika kesi hii), kupitia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alishinda baada kupata kura
56,196 dhidi ya mpinzani wake wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Batilda
Salha Buriani aliyepata kura 37,460.
Wajibu rufaa walijulikana kama wapiga kura waliosajiliwa na ambao
walikuwa ni wanachama wa CCM hawakuridhishwa na matokeo, hivyo
walifungua kesi ya kupinga matokeo katika Mahakama Kuu ya Arusha,
waliwasilisha ushahidi na kweli matokeo ya uchaguzi yalibatilishwa.
Hoja yao ya msingi (locus stand) iliyowafanya wafungue kesi ilikuwa
kwamba mwomba rufaa (Godbless Lema) alitamka maneno yasiyo ya
kistaarabu wakati wa kampeni, ambapo maneno hayo yanaweza kutafsiriwa
kuwa ni ya kufedhehesha, na ya kibaguzi yakiwa na lengo la kuleta
ubaguzi wa kidini, kijinsia na ubaguzi wa kimakaazi mambo ambayo
yalisababisha wapiga kura wasimchague Dk. Batilda Salha Burian.
Wajibu rufaa katika kesi hiyo walikuwa na mashahidi 14, pamoja na
waleta maombi ya kesi, wakati muomba rufaa alikuwa na mashahidi wanne
akiwemo yeye. Mwanashei Mkuu wa Serikali aliyeunganishwa kama sehemu
muhimu, hakuwa na shahidi yeyote.
Baada ya kusikiliza pande zote kupitia kwa mawakili wao, jaji aliona kuwa muomba rufaa alitenda mambo yaliyolalamikiwa.
Jaji wa Mahakama Kuu hakujielekeza vizuri kuhusu sheria za uchaguzi na
gharama zake pamoja na uwajibikaji wa wajibu rufaa na hivyo
alimwelekeza Msajili wa Mahakama Kuu ya Arusha kumwandikia mkurugenzi wa
uchaguzi wa taifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kifungu cha
114(1)-(7) na kifungu cha 343 (kama kilivyorekebishwa mwaka 2002, ili
muomba rufaa awekewe vikwazo vya kukosa sifa za kugombea baada ya
kubatilisha matokeo; muomba rufaa hakukubali, hivyo alikata rufaa.
Katika rufaa hii, mawakili Alute Mughwai na Moldest Akida walikuwepo
Mahakama ya Rufaa kama mawakili wa wajibu rufaa, huku Method Kimomogoro
na Tundu Lissu wakiwa mawakili wa muomba rufaa (Lema) katika mahakama
hii. Mwanasheria Mkuu wa serikali aliwakilishwa na mwanasheria wa
serikali Timon Vitalis.
Mwomba rufaa alitoa sababu 18 kupinga hukumu ya Arusha. Tulisoma kwa
uangalifu na kwa umakini msimamo wa wajibu rufaa wa kuleta kesi hii
(maombi haya). Hatukuona kama ni suala la msingi kwa kuwa suala lenyewe
halikuwa wazi zaidi, hii ni kwa sababu msingi wa hoja ya kesi ni wa
muhimu katika kuanzisha kesi zozote za kisheria katika mahakama; kwamba
kuna kesi ya kujibu au haiko kisheria.
Kwa kuwa suala la hoja ya msingi ya uwepo wa kesi ni la umuhimu katika
uendeshaji wa kesi kama hizi, na kwa kuwa rufaa ya aina hii ni ya
kwanza katika mahakama hii, tuna mtazamo sahihi kuwa tunawajibika
kupitia kumbukumbu hizi ili tuweze kubaini kama waleta maombi
(walioshtaki) walikuwa na hoja ya msingi kufungua kesi mahakamani
kupinga matokeo au hapana.
Swali hili lilianzishwa na mawakili Timon Vitalis na Methos
Kimomogoro kama pingamizi la msingi. Katika kujibu suala hilo, wakili wa
wajibu rufaa Alute Mughwai alijielekeza katika kifungu cha 5.111(1) cha
sheria kuwa wajibu rufaa walikuwa kweli ni wapiga kura walioandikishwa
kihalali.
Aya ya pili ya malalamiko inasomeka: “Walalamikaji ni wapiga kura
walioandikishwa kupiga kura katika uchaguzi ambao matokeo yake
yanalalamikiwa, vivuli vya vitambulisho vyao vya kupigia kura vimewekewa
alama A( l-J)”. Ni kweli kwamba Wakili Alute Mughwai aliwasilisha
vitambulisho vya kupigia kura kuthibitisha kuwa walalamikaji walikuwa ni
wapiga kura walioandikishwa, hayo yalijiri mahakamani tarehe
06/09/2011.”
Bahati mbaya sana vitambulisho vya wapiga kura havikutolewa na
kukubaliwa na mahakama kama ushahidi kwa kanuni za kimahakama na taraibu
zake.
Jaji Mjuluzi aliridhika tu kwa kuonyeshwa vitambulisho vya wapiga
kura, na kujiridhisha kwa mujibu wa kifungu cha 111(1) (a) cha sheria ya
maamuzi ya Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Wiliam Bakari na wenzake
dhidi ya Chediel Yohane Mgonja na Mwanasheria Mkuu, katika kesi ya madai
namba 84 ya mwaka 1980, kwa uamuzi uliojikita katika kifungu cha 126
(a).
Lakini katika kesi hii hakuna ushahidi kwenye kumbukumbu za mahakama
kuonyesha kuwa wajibu rufaa walikuwa kweli ni wapiga kura
walioandikishwa kihalali. Kumbukumbu zina viambatanisho na kisheria
viambatanisho sio ushahidi ambao mahakama inapaswa kuugemea pasipo
kutiliwa shaka.
Katika kesi ya Sabry Hafidhi Khalfan dhidi ya Zanzibar Telecom Ltd
(Zantel) Zanzibar Kesi ya madai Na. 47 ya 2009 ambayo haikuripotiwa
mahakamani ilisema: “Tunapaswa kujua kwamba viambatanisho vilivyoletwa
na mlalamikaji au vilivyotolewa katika maelezo ya mlalamikiwa sio
ushahidi.
“Labda kwa faida ya sasa tutamke kwamba lengo lote la kuambatanisha
viambatanisho kwenye kesi ni kuwezesha pande zote kujua kesi
inayozikabili. Kwa hiyo wazo la kuzungumzia viambatanisho katika kesi
visichukuliwe kama ni ushahidi.”
Baada sasa kujiridhisha na tafsiri hiyo kuhusu hadhi ya viambatanisho
vinavyoletwa na utaratibu unaotumika kuvifikisha mahakamani kisheria,
tunapaswa tuangalie mpiga kura aliyeandikishwa ni yupi? Jibu linatolewa
chini ya kifungu cha 13,19 na 20 vikisomwa pamoja. Mpiga kura halali
aliyeandikishwa ni raia yeyote wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18
anayekidhi mahitaji ya kisheria.
Kwa kuzingatia hayo mtu anaandikishwa kuwa mpiga kura endapo tu
msimamizi wa uchaguzi au msaididi wake au ofisa yeyote aliyepewa jukumu
la kuandikisha katika eneo husika atakuwa ameridhika na vigezo na ofisa
anayetajwa atampa kitambulisho cha mpiga kura.
Mtu huyo baada ya kujiandikisha na kupewa kitambulisho anakuwa mpiga
kura halali. Kwa hiyo kisheria kitambulisho cha mpiga kura kilichotolewa
kihalali na maafisa waliotajwa ni uthibitisho wa halali wa mpiga kura
aliyeandikishwa. Kitambulisho hicho ni uthibitisho kwa mwenye nacho kuwa
ni mpiga kura halali.
Katika kesi hii, tumeonyesha kuwa Wakili Alute amejaribu kuonyesha
kuwa wajibu rufaa walikuwa ni wapiga kura halali kwa kuleta vitambulisho
vyao vya kupigia kura kwa jaji. Kwanza haisemwi wazi kwa nini Alute
“yeye mwenyewe” alipeleka vitambulisho vya kupigia kura kwa jaji; pili,
hata utaratibu wa “upelekaji” vitambulisho hivyo ni kinyume na
taratibu zinazojulikana za kupeleka viambatanisho na/au kumbukumbu
mahakamani.
Kawaida ushahidi huo, katika kesi hii, kitambulisho cha mpiga kura
kilipaswa kuwasilishwa na mpiga kura mwenyewe ambaye ndio mmiliki
halali. Tunataka kuweka wazi kiujumla kuwa sheria ya ushahidi lengo
lake ni kutoa ulinzi (au maelekezo yafaayo) ni kwa namna gani (ipi) na
ni vipi ushahidi unavyopaswa kuchukuliwa na kupelekwa mahakamani ili
kuondoa au kupunguza mianya ya kutotenda haki.
Bila kuzingatia misingi hiyo ya kuulinda ushahidi, kiurahisi sana
mahakama inaweza kuangukia katika kile kinachoitwa Mahakama ya Kangaroo
(angalia Herman Henjewele dhidi ya kesi ya jinai Na. 164/2005
(haijaripotiwa); hata hivyo, kumbukumbu za mahakama hazionyeshi kama
wajibu rufaa walipatiwa fursa ya kuzungumzia kitu chochote chenye
uhusiano na kuvipeleka vitambulisho vya kupigia kura vinavyozungumzwa
hapa kwa utaratibu tuliouzoea.
Zaidi ya hayo yote vitambulisho hivyo vilirudishwa kwa wakili wao siku
ileile, kwa hiyo haviwezi kuzingatiwa kuwa ni sehemu muhimu ya
kumbukumbu za mahakama katika kesi hii ukizingatia pamoja na njia
iliyotumika kuviwasilisha mahakamani. Kwa mtiririko huu wa kisheria
tunajiridhisha kuwa hakukuwa na ushahidi au kumbukumbu kuonyesha kuwa
wajibu rufaa hawa walikuwa wapiga kura halali kwa makusudi ya kifungu
cha 111(1)( a) cha sheria.
Potelea mbali tuchukulie kuwa wajibu rufaa walikuwa ni wapiga kura
halali, tujiulize je walikuwa na haki ya msingi wa kusimamia (au hadhi
yao kisheria) ili kuweza kupinga matokeo ya uchaguzi kwa misingi ya
maneno yasiyo ya kistaarabu ambayo muomba rufaa (Lema) inasemekana
aliyatamka wakati wa kampeni?
Tumeonyesha dhahiri kuwa Wakili Alute alikubaliana na utafiti wa
Mujuluzi J kuhusiana na hukumu ya ya kesi ya Mgonja, lakini kwa upande
mwingine Wakili Timon Vitalis, Method Kimomogoro, na Tundu Lissu
walipinga kwa nguvu zote hapa kwenye Mahakama ya rufaa, na hoja yao ya
msingi ilikuwa “suala hili liko kinyume cha sheria”.
Sheria inasema, suala hili sio utashi wa kijamii kwa mwenendo wa kesi
kisheria chini ya kifungu cha 26 (6) cha Katiba, kwa hiyo haki ya msingi
ya kusimamia kimahakama mtu anayopaswa kuonyesha ni kuwa haki zake
ziliingiliwa au maslahi yake yalikiukwa na matokeo yake yanapaswa
yaonekane (athari ionekane), kwa hiyo mpiga kura hana haki ya kupinga
matokeo ya uchaguzi kwa kuwa haki zake na maslahi yake hayakukiukwa au
kuingiliwa. (Haki za mpiga kura ni kuandikishwa, kupiga kura na
kuhakikisha kura yake ilihesabiwa, je wajibu rufaa kati ya hizo haki zao
ipi ilikiukwa?). Kifungu cha 111(1) kinasomeka: 111(1) Matokeo ya
uchaguzi yanaweza kupingwa na mmojawapo kati ya hawa wafuatao, (a)Mpiga
kura aliyepiga kura kihalali, au alikuwa na haki ya kupiga kura kwenye
uchaguzi unaobishaniwa.
Kwanza tunaomba kueleza pasipo shaka kuwa sheria ya msingi wa
kusimamia hoja iko katika sheria za kawaida, na inatumika katika
mahakama zetu kwa mujibu wa kifungu cha 2(3) ya ulazima wa kisheria na
matumizi ya sheria kifungu cha 358 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 ili
kuweza kuendana na sheria ya misingi ya kuwa na hoja katika hali kama
hii inapojitokeza. Soma Lujuna Shubi Ballonzi, Senior dhidi ya Bodi ya
Wadhamini ya Chama cha Mapinduzi (1996) (tlr 203).
Kwa sasa katika Tanzania imepanuliwa zaidi ili iweze kuendana na
utashi wa jamii kifungu 26 (2) cha Katiba, kwa hiyo raia wa nchi hii ana
hoja ya msingi kusimamia anaposhtaki kwa masuala yenye manufaa
kijamii.
Na ulazima wa kisheria unategemea na haki inayotafutwa na taathira
yake (madhara) yake kijamii. Katika Kesi ya Christopher Mtikila dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali [1995] TLR 31 Lugakingira J, alizingatia
ulazima wa kufuata sheria katika suala hilo na manufaa ya kijamii,
akasema: “Pamoja na ulazima wa kuzingatia sheria kwa manufaa ya umma,
mahakama hii haikatai ukweli kuwa mlalamikaji ana manufaa binafsi na
kesi hii.”
Alienda mbali zaidi akasema: “Ulazima wa kisheria katika kesi hii sio
kuonyesha/kuridhisha udadisi wa watu, lakini sheria zimewekwa ili
kuisaidia mahakama iweze kutoa nafuu kwenye jamii yote au kikundi fulani
cha jamii.
Katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Chama cha
Congress cha Malawi, kesi ya madai Na.22 ya Mwaka 1996, Mahakama ya
Rufaa ya Malawi ilionyesha msingi wa kusimamia haki kisheria na ilisema
hivi: Suala la hoja ya msingi wa kesi, ni suala la kisheria, ni masuala
ya utawala bora tukizingatia kuwa sio kila mtu anaweza kufungua kesi
kama yeye sio sehemu ya suala linalobishaniwa. Hii ni kusema kuwa ni
lazima awe sehemu ya jambo linalobishaniwa kisheria.
Katika kesi hii na maamuzi; kwamba iwe wajibu rufaa walikuwa au
hawakuwa wapiga kura halali kwa mujibu wa kifungu cha 111 (1)( a) cha
sheria kinachompa mtu haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki
zake hazikukiukwa na maslahi yake kuingiliwa.
Tumelitafakari sana suala hilo na hivyo tunapenda kusema: kwanza
masuala ya kesi za uchaguzi sio manufaa kwa umma, ingawa yana umuhimu
mkubwa sana kwa umma. Hii ni kwa sababu pengine haki inayotafutwa
haiwezi kuinufaisha jamii yote kwa ujumla wake. Pili, kesi ilifunguliwa
chini ya kifungu cha sheria na 26 (2 cha Katiba kinachoruhusu kila raia
kuleta malalamiko kisheria kwa manufaa ya umma.
Kifungu hicho cha Katiba kinasomeka: “Kila mtu kwa mujibu wa sheria anaweza kufungua kesi kulinda Katiba.”
Kwa kuwa kesi ya uchaguzi sio kwa manufaa ua umma, kisheria hatusomi
kifungu hicho kwani tutakuwa tumekiuka kifungu kinachohusu ‘haki ya
msingi ya kusimamia hoja’ [locus standi]. Tunaona kwa mtazamo wetu,
kifungu cha 111(1) (a) cha sheria kinatoa haki kwa mpiga kura ambaye
haki zake zimekiukwa au maslahi yake kuingiliwa.
Kwa hiyo kwa kesi hii ukiukwaji kama ulifanyika, basi mlalamikaji wa
kwanza anapaswa awe mgombea mwenyewe ambaye haki zake zilikiukwa. Na ili
kukipatia kifungu hiki tafsiri pana, yeye ndiye ana haki zaidi hata
kama haki zake hazikukiukwa angetetea vizuri kanuni na hoja ya kusimamia
misingi ya uwepo wa kesi ya kujibu [locus stand]. Hatuko tayari
kukiuka kanuni hii. Hivyo, tunakubaliana na hoja za Timon Vitalis,
Method Kimomogoro na Tundu Lissu kwenye suala la “wapiga kura halali”.
Kwa mtazamo huo huo, tunathibitisha pasipo shaka kuwa kesi ya Mgonja
ilihukumiwa kinyume, ilitoa tafsiri potofu ya ‘hoja ya msingi ya uwepo
wa kesi ya kujibu’.
Tunasema hivyo kwa kuwa hatufikirii kwamba mahakama iliruhusu kila
mpiga kura yeyote bila kuzingatia mahali alipojiandikisha na kupiga kura
anaweza kupinga matokeo ya uchaguzi wowote, wa jimbo lolote mahakamani
katika nchi hii. Utakuwa ni ujinga.
Katika kesi ya Grey dhidi ya Pearson (1857) 6 HLC 61 ilieleweka: “Kama
tafsiri ya maneno inaweza kupelekea ujinga na/au upumbavu wa aina
fulani au uhusiano wa maneno yanayopingana au tabia ya kubadilika
badilika, kukosa msimamo hali hiyo inaweza kuepukwa ili kutojiweka
katika ujinga/upumbavu na kuonekana hatuna msimamo.”
Kwa mtazamo huo, kwa utulivu kabisa tunasema kuwa wajibu rufaa
hawakuwa na hoja ya kusimamia misingi ya uwepo wa kesi ya kujibu (locus
stand) katika kesi iliyoletwa katika Mahakama ya Rufaa. Hiyo peke yake
inatosha na kumpa mwomba rufaa haki.
Rufaa imeshinda na tunatengua hukumu ya Mahakama Kuu kwa amri ya
Mahakama ya Rufaa, tunamtangaza muomba rufaa kuwa mbunge wa jimbo la
Arusha Mjini. Wajibu rufaa watapaswa kulipa gharama za muomba rufaa
pamoja na mawakili wake wote wawili.
Imetolewa Dar es Salaam, Decemba 19, 2012. Mbele ya Jaji N.P Kimaro, B.M Luanda na S.A. MASATTI.
0 comments:
Post a Comment