PATA HABARI/MAKALA ZA UHAKIKA

+255-767-402-396

KAMISHENI YA AFRIKA KUSIMAMIA USIKILIZAJI WA KESI ZA MAUAJI YA KIMBARI RWANDA


 Na Nicodemus Ikonko, Hirondelle, Arusha
 Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imehitimisha majadiliano na Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) ili kusimamia usikilizaji wa kesi za mauaji ya kimbari zinazopelekwa kusikilizwa nchini Rwanda.
‘’Hali iliyopo sasa ni kwamba ICTR kupitia ofisi ya Msajili imeshahitimisha majadiliano na ACHPR kusimamia usikilizaji wa kesi,’’ Msemaji wa Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, Roland Amossouga aliliambia Shirika la Habari la Hirondelle Jumanne.
Aliongeza kwamba,’’Hati ya makubaliano hayo itatiwa saini hivi karibuni na baada ya hapo ACHPR ndipo itaanza rasmi kazi yake ya kusimamia kesi ya (Jean) Uwinkindi nchini Rwanda.’’
Wafanyakazi wawili wa ICTR waliteuliwa Aprili mwaka huu kama wasimamizi wa muda wa kesi ya Uwinkindi, huku ACHPR ikisubiriwa kukamilisha makubaliano na ICTR kufanya kazi hiyo. ACHPR ina majukumu ya kulinda na kukuza haki za binadamu ikiwa ni miongoni mwa kazi zake. 
Wakati ukitolewa uamuzi wa kuhamishia kesi ya Uwinkindi kwenda Rwanda Juni 2011, Majaji walimwelekeza Msajili wa Mahakama ICTR kuingia katika mkataba wa maandishi na ACHPR ambao utaeleza wazi maslahi, fedha zinazohitajika na mambo mengine muhimu ambayo yatafanya taasisi hiyo kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa mujibu wa majaji ‘’ACHPR itatakiwa kuwasilisha ripoti ya mara kwa mara kila baada ya miezi mitatu juu ya hali ya mwenendo wa kesi kwa Rais wa ICTR kupitia kwa Msajili wake, wakati kesi itakapoanza kusikilizwa hadi hapo itakapohitimishwa ikiwa ni pamoja na hatua ya rufaa kwa mshitakiwa na pia katika hatua ya kusimamia adhabu itakayotolewa, kama itakuwepo.’’
Majaji waliridhika kuwa hatua ya Kamisheni hiyo kusimamia mwendendo mzima wa kesi utatoa hakikisho kwamba ukiukwaji wowote wa haki ya mshitakiwa katika mwenendo wa kesi yake utapelekwa mbele ya Rais wa ICTR mara moja ili hatua za kurekebisha zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kufikiria kuiondoa kesi hiyo kusikilizwa mbele ya mahakama za Rwanda.
ICTR tayari imeridhia kesi nane kwenda kusikilizwa nchini Rwanda. Uwinkindi, ambaye ni mchungaji alihamishiwa nchini Rwanda Aprili 19, 2012, akiwa ni mshitakiwa wa kwanza wa ICTR kesi yake kwenda kusikilizwa nchini humo.
Nje ya Uwinkindi, kesi nyingine zilizohamishiwa nchini Rwanda ni pomoja na mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa na ICTR na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe, watuhumiwa sita ambao bado wanasakwa, wakiwemo mameya watatu, polisi mmoja, afisa wa zamani wa jeshi na meneja mmoja wa mgahawa. Hata hivyo kesi nyingine mbili bado zipo mbele ya Mahakama ya Rufaa zikisubiri uamuzi.

NI/FK
© Hirondelle News Agency
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments: